MSAFARA WA DC UMESHAMBULIWA NA WATU WASIOJULIKANA



Mkuu wa Wilaya ya  Karagwe, Godfrey Mheluka 

Karagwe. Msafara wa Mkuu wa Wilaya ya  Karagwe, Godfrey Mheluka uliokuwa katika operesheni ya kuwaondoa watu wanaodaiwa kuvamia maeneo ya wafugaji katika Kijiji cha Kashanda, Kata ya Nyakahanga, umeshambuliwa na watu wasiojulikana.

Katika shambulizi hilo lililotokea leo Agosti 29 saa tano asubuhi, diwani wa Nyakahanga, Charles Bechumila amejeruhiwa na amepelekwa katika Hospitali Teule ya Nyakahanga.

Mkuu wa wilaya hiyo, Mheluka amesema bado hajawa sawa, hivyo atazungumzia tukio hilo  baadaye.

Ofisa Tarafa ya Bugene Nyaishozi, Rozaria Christian amesema walikuwa kwenye operesheni halali na wakulima hawana na taarifa.

Amesema baada ya kuwakamata wawili ndipo kundi la watu lilijitokeza likionyesha kuwa lilijiandaa kuwashambulia.

Christian amesema watu kadhaa wamekamatwa wakituhumiwa kuhusika kumjeruhi diwani huyo.

Shuhuda wa tukio hilo aliyekuwa kwenye msafara huo amesema baada ya kufika kijijini humo aliwakuta baadhi ya watu wakilima na walikamatwa.

Baada ya kukamatwa amesema kundi hilo la watu liliwashambulia kwa mishale na mikuki hivyo walikimbia ndipo diwani alipojikwaa na kuanguka na watu hao wasiofahamika walimshambulia kwa  kumchoma mishale na kumkata kwa panga.

Comments