Mauaji gesti kizungumkuti


VYUMBA VYA NYUMBA ZA KUFIKIA WAGENI. PICHA: MITANDAO

TUKIO la watu wawili kukutwa wamekufa wakiwa uchi na kufungwa kamba miguuni na mikononi katika nyumba ya wageni jijini hapa, limeonekana kuvichanganya vyombo vya ulinzi na usalama huku serikali ikionekana kukosa majibu.

Sakata hilo liliibuka jana katika mkutano  maalumu  wa Baraza la Madiwani wa Jiji la Tanga lililokuwa na lengo la kupitisha na kukubali hesabu za mapato na matumizi kwa kipindi cha mwaka 2016/17.

Diwani wa Marungu, Mohamed Mwambeya (CCM), pamoja na mambo mengine, alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kudhibiti matukio ya mauaji kwenye nyumba za wageni kama lile ya hivi karibuni.

Mwambeya alivitaka vyombo vya usalama kuhakikisha nyumba za wageni, pamoja na mambo mengine, zinakidhi vigezo vikiwamo vya ulinzi na mazingira salama kwa wanaozitumia. Alisema jambo hilo ni muhimu hasa katika kipindi hiki ambacho jiji linakabiliwa na wageni wa aina mbalimbali kutokana na fursa za uwekezaji zilizopo.

Meya wa Jiji la Tanga, Mhina Mustapha, kutokana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama kuwa wajumbe katika mkutano huo, ana imani wamelichukua na watalifanyia kazi ili kuhakikisha si usalama pekee lakini pia ni kulinda heshima ya utulivu wa jiji.

Mustapha alisema suala la ulinzi na usalama ni mtambuka na kuwataka viongozi na wakazi wa jiji kuhakikisha kila mmoja anakuwa mlinzi kwenye eneo lake ili kudhibiti vitendo viovu.

Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa, alipoulizwa kuhusiana na mauaji hayo, alikiri kukosa majibu lakini alisisitiza kupatikana na kuchukuliwa hatua stahiki watu waliohusika kwa mujibu wa sheria.

Mwilapwa  alisema tukio la kuawa watu wawili lililotokea mwishoni mwa wiki jijini hapa, limeamsha ari mpya na kwamba mkakati wa kudhibiti uhalifu utaimarishwa.

Hata hivyo alisema ulinzi ni jukumu la kila raia na kubainisha kuwa akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, anahitaji sana ushirikiano.

Alisema mauaji hayo bado ni kizungumkuti kwa kuwa yanaweza kufanywa na raia wa Tanzania au watu kutoka nje ya nchi, jambo alilodai kuwa licha ya kujizatiti, jamii ni nguzo muhimu kwa kuwa jiji la Tanga na Mkoa kwa ujumla uko mpakani na nchi jirani pamoja na uwepo wa Bahari ya Hindi.

Mwilapwa alisema hali hiyo inasababisha mianya mingi kwa watu kuingia kinyemela na kutekeleza uhalifu.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedicto  Wakulyamba, hadi sasa hakuna mtu anayeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo na kwamba jeshi bado linaendelea na uchunguzi.

Awali, alisema Septemba 25, majira ya saa mbili asubuhi, mhudumu wa nyumba ya wageni ya Bomai Inn iliyoko mtaa wa Umba, aligundua miili ya watu wawili wanaume katika chumba namba 303 wakiwa wamekufa na kufungwa kamba miguuni na mikononi.

Comments