Talaka 546 zaripotiwa mahakamani











TAKWIMU zilizokusanywa na asasi za kiraia za kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto Zanzibar, zinaonesha kwamba talaka 546 zimeripotiwa katika Mahakama za Kadhi Unguja na Pemba katika kipindi cha mwaka mmoja tu kuanzia Januari hadi Agosti mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa na asasi hizo, ikiwemo Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) na Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (Zafela), zinaonesha kwamba wingi wa talaka hizo hakuna mgawanyo wa mali, uliofikiwa kwa wanandoa hao huku wanawake wakiendelea kuteseka kwa kuachiwa familia ya watoto.
Mkurugenzi wa Tamwa Zanzibar, Mzuri Issa alisema kesi zilizotolewa uamuzi ni 75 wakati kesi zinazoendelea Mahakamani ni 471. Alitaja baadhi ya athari kubwa katika utoaji wa talaka holela ni kuwepo kwa tatizo la utelekezaji wa watoto na kukosa matunzo na hatimaye wengine kukosa haki ya msingi ya Elimu.
Kwa mfano, alisema jumla ya kesi za matunzo ya watoto 22 zinaendelea mahakamani ambazo ni matokeo ya talaka. Wakitoa mapendekezo yao kupunguza tatizo la wingi wa talaka, Dk Mzuri alisema wakati umefika sasa kwa Ofisi ya Mufti na taasisi nyingine za kidini, kutoa mafunzo kwa wanandoa kabla ya kuoana.
Alisema katika mfumo wa sasa, wanandoa wengi wanaingia katika ndoa, lakini kwa bahati mbaya hawajui majukumu yao na fursa na haki zinazopatikana katika ndoa hiyo ikiwemo wakati itakapovunjika.
Akitoa mfano, alisema Malaysia yenye idadi kubwa ya wananchi wafuasi wa dini ya Kiislamu, hupewa mafunzo kwa watu wanaotarajiwa kufunga ndoa kwa muda wa siku tano kabla ya ndoa na Indonesia mafunzo hufanyika kwa wiki nzima na kulipiwa na serikali, ambapo wanandoa wanapofaulu hukabidhiwa cheti na kuruhusiwa kuingia katika utaratibu wa ndoa.

Comments