Mwanaume mmoja aliyefahamika kwa jina la Joseph Sahni, mkazi wa kijiji cha Nzonza Kata ya Salawe mkoani Shinyanga amefariki dunia akiwa nyumbani kwa mganga wa kienyeji wakati akipatiwa matibabu ya nguvu za kiume.

Sahni (60) alikutwa na mauti baada ya kuwekewa dawa ya unga kwenye tundu la sehemu zake za siri, kisha kusukumizwa kwa kupampiwa na pampu ya baiskeli.
Tukio hilo lilitokea Jumapili saa 10:00 jioni, ambapo Sahni baada ya kupatiwa matibabu hayo, alianza kutokwa damu nyingi sehemu zake za siri kisha kuishiwa nguvu na kupoteza maisha.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, Kamanda Simon Haule, amethibitisha taarifa hizo akisema kuwa Jeshi lake linamshikilia Mganga huyo wa kienyeji, Robert Mkoma, kwa tuhuma za mauaji, na baadaye atafikishwa mahakamani baada ya taratibu kukamilika.
“Natoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kuacha tabia ya kuendekeza kukimbilia kwa waganga wa kienyeji kutafuta tiba, waende kwenye vituo vya afya au hospitali kufanyiwa uangalizi na kupewa matibabu sahihi,”amesema Kamanda Haule.
Chanzo: NIPASHE
Comments
Post a Comment