Marekani yajitayarisha tena na kimbunga Nate


Kimbunga Nate kimepata nguvu zaidi wakati kinaelekea katika rasi ya Yukatan nchini Mexico baada ya kusababisha mvua kubwa katika eneo la Amerika ya kati na kusababisha vifo vya karibu watu 21.

Watabiri wa hali ya hewa wamesema upepo huo mkali na mvua huenda ukafika katika pwani ya ghuba ya Marekani kama kimbunga mwishoni mwa juma.

Maafisa wa Louisiana na Mississippe wametangaza hali ya hatari na Louisiana wameamru baadhi ya watu waondolewe katika maeneo ya pwani na visiwa vya vizuwizi kabla ya kutarajiwa kuwasili kwa kimbunga hicho leo Jumamosi usiku ama mapema Jumapili. Uondoaji wa watu ulianza katika maeneo ya nje baharini katika maeneo yanayochimbwa mafuta katika eneo hilo la ghuba.

Upepo mkali na mvua nyingi huambatana na vimbunga

Serikali ya jimbo la Mississippi imesema itafungua vituo 11 vya kuhifadhi watu katika maeneo nje ya eneo la karibu la pwani, ambapo mabasi yametayarishwa kwa ajili ya watu ambao hawana magari.

Kituo kinachohusika na masuala ya vimbunga nchini Marekani kimeonya kwamba kimbunga Nate kinaweza kupandisha viwango vya bahari kwa zaidi ya futi nne hadi saba , mita 1.2 hadi mita 2.1 , kutoka mji wa Morgab, Louisiana , hadi mpaka kati ya Alabama na florida. Kimbunga hicho tayari kimesababisha mafuriko makubwa katika eneo kubwa la Amerika ya kati.

Kituo hicho kimeongeza mji wa New Orleans na ziwa Pontchartrain katika orodha ya hivi karibuni kabisa ya tahadhari kwa kimbunga hicho.

Comments