Mwalimu ajiuwa kwa kwa kujichinja koromeo


Sumbawanga. Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Mtenga wilayani Nkasi, Leonard Mwipugi (29) amejiua kwa kujichinja koromeo akiwa nyumbani kwake.

Taarifa zilizotolewa na Mratibu wa Elimu Kata ya Mtenga, Hebron Mwafungo zimeeleza kuwa mwalimu huyo amekutwa akiwa amekufa baada ya kujichinja nyumbani kwake muda wa saa sita mchana leo Jumamosi.

Amesema kuwa mwalimu huyo alikwenda kazini kwake na saa 5 asubuhi alirejea nyumbani na hakumkuta mkewe na baada ya muda walipata taarifa kuwa mwalimu huyo amekutwa amekufa baada ya kujichinja koromeo chumbani kwake.

Amesema kuwa mwalimu huyo alikua akiishi na mdogo wake nyumbani hapo na alipofika alimtuma mdogo wake mbali kidogo ya nyumba hiyo na baada ya kurudi aliona damu na baada ya kuchungulia chumbani alikuta kaka yake amefariki dunia kwa kujichinja koromeo na kutoa taarifa kwenye uongozi wa kijiji hicho.

Amesema baada ya kumdodosa mdogo wa marehemu huyo alidai kuwa kaka yake siku za nyuma alikua na mgogoro na mkewe lakini ulikwisha ila anahisi kitendo cha mkewe kuondoka nyumbani na kwenda mjini Namanyere huenda jambo hilo lilimkasirisha na kuchukua hatua hiyo ya kujichinja.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando amesema chanzo cha kifo hicho bado hakijajulikana lakini polisi wanaendelea na uchunguzi ili kubaini kilichomsibu mwalimu huyo kiasi cha kuchukua maamuzi ya kujiua kikatili namna hiyo

Comments