Ubunifu wa Makonda waimarisha Jeshi la Polisi Dar es Salaam

Makonda akabidhi magari 18 kwa jeshi la polisi Dar es Salaam Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda leo amekabidhi Magari ya kisasa 18 kati ya 26 yaliyopelekwa Mkoani Kilimanjaro yakiwa Mabovu kwa ajili ya kufufuliwa.

Magari hayo yalipelekwa Kilimanjaro yakiwa yamebebwa kutokana na ubovu lakini sasa yanarejea Dar es Salaam yakiwa mazima na mwonekano kama magari ya UN ambapo yatakuwa na uwezo wa kubeba Askari 11 wakiwa wamekaa na silaha zao.

Akikabidhi magari hayo kwa Jeshi la Polisi leo Makonda amesema yataenda kuhudumia wananchi kwa kuimarisha ulinzi na usalama jijini Dar es Salaam. Amesema kuwa kilichomgusa kuboresha Jeshi la Polisi ni baada ya kuona askari wakifanya kazi katika mazingira magumu na wakati mwingine kuvamiwa na majambazi kisha kuuawa na kuporwa silaha.

Aidha Makonda ameishukuru kampuni ya Rajinder Motors Ltd (RSA) kwa kumuahidi kutengeneza magari 56 ya Polisi Dar es Salaam bila kutumia fedha za serikali. Makonda ametumia makabidhiano hayo kutuma salamu kwa majambazi, vibaka na wale wenye nia ya kuvuruga amani na usalama kuwa kiama chao kimefika.

Amesema alipotangaza mpango wa kufufua Magari yaliyokufa wapo waliombeza lakini sasa wanajionea magari yakiwa mapya. Makabidhiano hayo yameshuhudiwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mngwira, Kamanda wa Polisi kanda Maalumu ya Dar ea Salaam Lazaro Mambosas na viongozi wengine wa vyombo vya ulinzi na usalama ambapo wamempongeza Makonda kwa ubunifu mkubwa alionao.

Comments