SASA TUFANYE UTAFITI DOGO JANJA NA IRENE UWOYA

February 6, 2015 Ommy Dimpoz aliitikisa mitandao ya kijamii Bongo mara baada ya kuposti katika ukurasa wake wa Instagram akiwa na aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu.



Katika picha moja na Wema Sepetu inaweza kuwa stori ya kawaida ila wakati ulifanya kitendo hicho kuwa stori ya aina yake yenye kusisimua zaidi, wakati kwa maana ipi?.

Kipindi Ommy Dimpoz anatoa picha hiyo Wema alikuwa ametoka kuachana na aliyekuwa mpenzi wake ambaye ni Diamond Platnumz, yeah!! tunafahamu kuwa ushemeji hauna kikomo lakini kwa picha zile ilionekana ni kama zimevuka mpaka wa ushemeji.

Maswali yakawa ni mengi kutoka kwa mashabiki wao ni kweli Ommy na Wema wameamua kuanzisha uhusiano licha ya ukweli kwamba alikuwa ni rafiki wa karibu na Diamond? si kitu cha kawaida.

May 12, 2015 mashabiki walipata ukweli wa kile kilichokuwa kikiendelea kati ya Ommy Dimpoz na Wema Sepetu, ukweli ni kwamba picha zile zilikuwa ni katika utengenezaji wa video ya Dimpoz ‘Wanjera’ ambayo ilitoka tarehe hiyo.

Hata hivyo wachambuzi wa mambo katika upande wa muziki wanadokeza kuwa ngoma hiyo haikuwa na nguvu kubwa ukilinganisha ngoma nyingine za Ommy Dimpoz za hapo awali licha ya kutengenezewa ‘kiki’ hiyo, wanadai tukio hilo lilimeza hata ngoma yenyewe.

Dogo Janja na Irene Uwoya

Kuanzia weekend iliyopita hadi sasa wametawala mitandao kwa hapa Bongo kwa kile kinachodaiwa wamefunga ndoa, licha ya taarifa za awali kuwa na usiri mkubwa na kuibua baadhi ya maswali, November 3 mwaka huu (juzi) ndipo Dogo Janja alithibitisha kufunga ndoa na Irene Uwoya.

July mwaka huu ndipo pia taarifa zilianza kuibuka kuwa wawili hao wanatoka kimapenzi mara baada ya kuonekana Jijini Mwanza wakiwa pamoja, hata hivyo wote wawili walikuwa wakikanusha hilo pindi wanapoulizwa na vyombo vya habari.

Msanii Madee ambaye ni mlezi wa Dogo Janja alipoliuzwa na U–Heard ya Clouds Fm kuhusu hilo alieleza kutotambua uhusiano wao.

“Sijawahi kuwaona wakija pamoja home ila anasikia kama unavyosikia wewe kuwa ni wapenzi, ila taarifa hizo hazipo rasmi pia nitafatilia kujua kuhusu suala hilo ila hata ikiwa kweli kwani kuna tatizo?” alisema Madee.

Muda unasafiri mbio kama mwanga ndani ya chumba chenye giza, hatimaye sasa Dogo Janja na Irene Uwoya inaelezwa ni mume na mke. Naomba kurudia tena, hatamiye Dogo Janja na Irene Uwoya inaelezwa ni mume na mke, weka nukta hapo.

Tuwajadili Kidogo

Hadi sasa kuna watu ambao hawaamini iwapo kweli wamefunga ndoa na wengine wanaamini ila mimi sipo katika makundi hayo mawili. Wapo ambao wanachukulia kama kiki, mathalani ni kiki kweli, binafsi nitawapongeza kwani wamefanikiwa kwa asilimia zote.



Kwa wiki hii ikiangalia video zinazotrend katika mtandao wa YouTube Tanzania, stori za wawili hawa zimechukua nafasi kubwa sana, hadi siku ya jana jumla ya video 14 zilikuwa trend ni kuhusu ndoa ya Dogo Janja na Irene Uwoya.

Hata hivyo kuna mambo mawili ambayo yanatengeneza maswali, mosi; Usiri wa sherehe yao, vyombo vya habari na watu wake hawakupata nafasi kushuhudia hilo, pia idadi kubwa ya wasanii hawakupata fursa hivyo, kwani Dogo Janja hana marafiki wa rika lake katika muziki wake, vipi kuhusu Irene Uwoya?.

Pili; nimesikiliza kwa makini maelezo ya mama mzazi wa Dogo Janja akieleza ni kwanini hakuhudhuria katika ndoa ya mwanaye, pia nimesikiliza kwa makini zaidi maelezo ya Dogo Janja aliyoyatoa kuhusiana na hilo. Wote wapo sahihi ila kwa taratibu zetu za kiafrika au Tanzania kuna jambo/kitu kinakosekana katika majibu yao, tuachane na hilo.

Nimekumbuka Jambo

Kabla sijaeleza nilichokumbuka, nafurahi kukumbuka usemi wa mchekeshaji wa kundi la Orijino Komedi, Mpoki ambaye alisema mapenzi yana nguvu kuliko breakdown.

Nimekumbuka namna stori za kimahusiano kati ya wasanii kwa wasanii au watu maarufu zinavyokuwa na nguvu katika vyombo vya habari na mitandao duniani kote. Miongoni mwa stori za kimahusiano katika tasnia ya muziki Bongo zilizochukua nafasi hivi karibuni ni ile ya Diamond na Hamisa Mobetto, Jux na Vanessa Mdee, Nuh Mziwanda na mkewe.

Drama zilizokuwepo wakati kuna tetesi Diamond amezaa na Hamisa Mobetto kabla ya yeye kuja kukubali na hata alipofanya hivyo ni stori iliyouza sana katika vyombo vya habari na mitandao. Stori ya Vanessa na Jux kuachana pamoja na ile Nuh na mkewe nazo zilipewa nafasi kubwa.

Utafiti Uchukue Nafasi

Juzi katika show ya Fiesta iliyofanyika Dodoma nilipendezwa na ubunifu wa Ben Pol kumpandisha jukwani Ebitoke ambaye walidaiwa kuwa wapenzi, wengine wakisema ni kiki na hata tetesi za kugombana/kuachana kwao ilikuwa stori pia.

Ben Pol na Ebitoke wametumia ipasavyo kile walichokitengeneza, iwe ni kiki au mahusiano lakini katika show walichofanya ni faida kwao kiuchumi na kisanaa, twende pole pole.

Utafiti ninaotaka ufanyike ni kujua ni wasanii wangapi wananufaika kiuchumi au kukuza biashara zao pindi wanapokuwa na stori kubwa kama aliyonayo Dogo Janja na Irene Uwoya kwa sasa.

Utafiti ufanyike bila kujali stori husika imepatikana katika mtindo upi, iwe ni kiki au mahusiano ya kweli (serious) kama ya Jay Z na Beyonce. Nimeona Dogo Janja ameweka video ya sherehe yake katika channel yake ya YouTube, sijajua iwapo channel hiyo imesajiliwa/kuweka katika mfumo wa malipo ila nafikiri kulikuwa na fursa kubwa ya kuuza video hiyo katika tv station.

Hivyo basi, nitamatishe kwa kuwaeleza watafiti wangu wamuhoji kila msanii/staa Bongo ambaye alishakuwa au kutengeneza stori kubwa za namna hii akieleza ni jinsi alivyonufaika nayo kiuchumi tu. Vigezo na Masharti vya utafiti huu ni kwamba vitu kama ‘nilifanikiwa kutangaza wimbo/video/filamu/ jina langu havitajuishwa.

Comments