Amuuwa rafiki yake kikatili kwa deni la 4,000/=

Image result for mshale
Mwanaume mmoja mkazi wa Mtaa wa Kilimahewa katika Halmashauri ya mji wa Bunda mkoani Mara, Paul Juma (38), ameuawa kwa kuchomwa mshale wa sumu na rafiki yake, baada ya kutokea ugomvi wa madai kati yao.

Imeelezwa kuwa ugomvi huo ulitokana na Muuaji kudai aongezewe tsh 4,000 kutokana na kumuuzia marehemu mabati manne chakavu kwa tsh 20,000.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Jafari Mohamed, jana Desemba 28, 2017 alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kumtaja mtuhumiwa kuwa ni Julius Mtoni (48) mkazi wa mjini Bunda na watu hao walikuwa ni marafiki.

Kamanda Mohamed amesema tukio hilo lilitokea mnamo Desema 26, 2017, majira ya mchana wakati watu hao walipokuwa wanakunywa pombe ya kienyeji maeneo jirani na kwa marehemu.

Taarifa kutoka Polisi wilayani Bunda imeeleza kuwa mnamo Desemba 25, 2017 marehemu alimuuzia mtuhumiwa mabati manne chakavu kwa makubaliano ya kila bati tsh 7,000.

Inadaiwa kuwa siku hiyo mtuhumiwa huyo alimpatia marehemu Sh. 20,000 taslimu na kukubaliana kuwa atalipwa kiasi kingine cha Shilingi 8,000 kilichobakia siku nyingine.

Ndipo Desemba 26, 2017 wakiwa wanakunywa pombe, marehemu alimdai mtuhukiwa amlipe Sh. 8,000 zilizokuwa zimesalia, lakini alimpatia Sh. 4,000 na ndio wakaanza kuzozana huku marehemu akishinikiza alipwe deni lake lote la tsh 8,000/=.

Polisi wamesema kutokana na kutokuelewana, marehemu alianza kumkaba mtuhumiwa, ndipo mtuhumiwa akakimbilia nyumbani kwake na kuchukua upinde na kumfyatulia mshale ambao ulimpata begani.

Polisi walisema kuwa baada ya marehemu kuchomwa mshale huo aliuvunja na kubakiza kipande cha mshale huo mwilini mwake na kukimbilia polisi, lakini alipoteza maisha kutokana na kutokwa na damu nyingi.

Chanzo:Nipashe

Comments