Kama mwaka 2017 ni meli basi ndio inakaribia kutia nanga, yaani mwisho wa safari. Zikiwa zimebakia siku zipatazo 21 kumaliza mwaka kuna mengi ya kuzungumza katika muziki wa Bongo Flava na wasanii wenyewe wanaofanya muziki huo.
Kabla ya kufika mbali naomba nieleweke hivi; vitu alivyofanya kwa mwaka huu hakuwahi kuvifanya katika miaka iliyopita, hivyo amepiga hatua katika maeneo fulani. Maeneo hayo ni tofauti sana ukilinganisha na wasanii wengine, sasa tusemaje zaidi ya kuwanyoosha?, twende pole pole.
Kolabo kubwa za kimataifa
Twende mbele twende nyuma, kwa mwaka huu ndio Diamond amefanya kolabo kubwa za kimataifa zaidi ukilinganisha na miaka mingine iliyopita.
Alifungua mwaka kwa kuachia kolabo ‘Marry You’ na msanii Ne-Yo kutoka nchini Marekani. Ngoma hiyo iliyotoka Feb 2, 2017 ilikuwa ikisubiriwa kwa kipindi kirefu tangu mwaka 2015 ambapo ilithibitika kuwa kuna kolabo ya wawili hao.
Wakati Diamond anakutana na Ne-Yo nchini Afrika Kusini kwenye tuzo za MAMA 2015 na taarifa za ujio wa kolabo ya kuanza kusikika iliaminika kuwa ni mwanzo wa kuanza kutangaza muziki wake dunia nzima kwani Ne-Yo ni msanii mkubwa duniani. Hilo amefanikiwa kulitimiza mwaka huu kwa kuachia ngoma hiyo.
Kutoa kolabo na Ne-Yo ilikuwa ni mwanzo wa kuwatafuta wasanii wakubwa duniani mara baada kutoa ngoma nyingi na wasanii wengi wakubwa wa Afrika kama Davido, Iyanja, Mr. Flavour, AKA, Mafikizolo, Tiwa Savage na wengineo.
Mara paap!!!, September 28, 2017 hii hapa, Diamond anaachia ngoma ‘Hallelujah’ na kundi la Morgan Heritage kutoka nchini Jamaica.
Kundi la Morgan Heritage ni kubwa sana nchini Jamaica, tangu kuanzishwa kwake mwaka 1994 limekuwa likifanya vizuri na hadi sasa wametoa albamu zaidi ya 15. Pia mwaka 2015 walishinda tuzo ya Grammy kupitia albamu yao ‘Strictly Roots’.
Kwa stori hiyo fupi ya Morgan Heritage utaona ni kwa jinsi gani ambavyo Diamond kiwango chake cha uimbaji kimekuwa kikubwa hadi kufikia hatua ya kufanya kazi na wasanii hao. Ni jitihada ambazo zinapaswa kutambuliwa na kuungwa mkono pasina shaka.
Baada ya kutoka Jamaica anarudi tena Marekani, safari hii anakutana na Rick Ross na wanatoa ngoma ‘Waka’ ambayo imetoa wiki hii. Kolabo hii haikupata kuzungumziwa sana kama ile ya Ne-Yo kwa sababu taarifa za ujio wake zimetoka kwa kipindi kifupi mno kisha yenyewe ikafuata.
Ujio wa biashara mbili
Kwa mwaka huu Diamond ameweza kuingiza sokoni bidhaa zake mbili, Chibu Perfume na Diamond Karanga.
Diamond ameamua umaarufu alionao kwa sasa kutopita bure badala yake akaamua kufanya nao biashara nyingine nje ya muziki kama wanavyofanya wasanii wengi duniani ambao wanamiliki kiasi kikubwa cha fedha.
Kwa mujibu Forbes Diddy na Jay Z wameongoza orodha ya wasanii wa hip hop wenye fedha zingi zaidi duniani, taarifa ya May mwaka huu inaonyesha Diddy ameingiza dola milioni 820 ndani ya mwaka mmoja, huku Jay Z akiingiza dola milioni 810.
Fedha hizo hazitokana na muziki pekee bali katika biashara nyingine walizowekeza, Diddy anaingiza fedha nyingi zaidi kupitia biashara zake kama vile Cîroc Vodka, Revolt TV, huku Jay Z akinufaika na kampuni zake za Tidal, Roc Nation, Roc Nation Sports na dili nyingine kupitia filamu anazofanya kupitia kampuni ya Weinstein Company.
Diamond naye anajaribu kupita njia hizo, unapotaka kuwa msanii wa kimataifa siyo tu kutoa ngoma kali na wale wa kimataifa na kushindana nao, suala la kiuchumi linakupa hadhi fulani pindi mnapokuwa pamoja, huwezi kujiita msanii wa kimataifa wakati ukikutana na wale wa kimaifa unakuwa mnyonge.
Diamond alianza mwaka kwa kuingiza sokoni manukato ‘Chibu Perfume’ kitu ambacho kilikuwa kigeni sana kwa hapa Bongo kwani wasanii wengi wamejikita katika biashara ya vitu kama nguo.
Kupitia Chibu Perfume Diamond anaungana na mastaa wengine duniani kama Nicki Minaj, Beyonce, Diddy, David Beckham, Kim Kardashian na wengine kufanya hivyo.
Hivi karibuni alikiri kuwa biashara hiyo ya karanga inamuingizia fedha nyingi zaidi kuliko ile ya manukato. Vyovyote itakavyokuwa, upende au uchukie, Diamond kwa mwaka huu, 2017 amefanya vizuri katika muziki na biashara kama wanavyofanya wasanii wengi wakubwa duniani. Naomba kuwasilisha.
Comments
Post a Comment