Mamake kiongozi wa al-Qaeda Osama Bin Laden amezungumza hadharani kwa mara ya kwanza , miaka saba baada ya kifo cha mwanawe mwaka 2011.
Alia Ghanem alifanya mahojiano na gazeti la The Guradian katika nyumba ya familia hiyo mjini Jeddah Saudia.
Aliambia gazeti hilo kwamba ,mwanawe alikuwa mwenye haya na mtoto mzuri lakini akapewa itikadi mbaya akiwa chuo kikuu.
Familia hiyo inasema kwamba mara ya mwisho kumuona Bin Laden ilikuwa 1999, miaka miwili kabla ya mashambulio wakati alipokuwa akiishi nchini Afghanistan.
Wakati alipogunduliwa kuwa mshukiwa mkuu wa ugaidi duniani, baada ya kuhamia nchini humo ili kupigana dhidi ya vikosi vya Sovieti vilivyovamia 1980.
''Tulikasirika sana , sikutaka matatizo hayo kutokea, kwa nini alibadilika na kuwa namna hiyo mara moja''? Bi Ghanem aliambia gazeti hilo, alipoulizwa alihisi vipi alipogundua kwamba mwanawe amebadilika na kuwa mpiganaji wa kijihadi.
Pia alisema kuwa kundi la Muslim Brotherhood ambalo mwanawe alihusika nalo wakati wa masomo lilikuwa kama madhehebu.
Familia ya Bin Laden imesalia kuwa familia maarufu zaidi nchini Saudia baada ya kujipatia utajiri mkubwa kupitia ujenzi.
Babake Bin Laden , Mohammad bin Awad bin Laden, alitalakiana na mkewe Alia miaka mitatu baada ya Obama kuzaliwa na alikuwa na jumla ya watoto hamsini.
Baada ya shambulio la 9/11, familia hiyo inasema kuwa ilihojiwa na serikali ya Saudia ambayo baadaye ilizuia usafiri wao.
Mwandishi wa habari Martin Chulov aliandika katika taarifa kwamba aliamini kwamba ufalme wa Ghuba ulimpatia ruhusa kuzungumza na Bi Ghanem kwa sababu maafisa waandamizi walitumai kwamba kiongozi huyo wa al-Qaeda alikuwa mtu aliyekataliwa na sio wakala wa serikali, kama vile wengine walivyodhania.
Nduguze bin Laden Hassan na Ahmad pia walikuwepo wakati wa mahoijiano hayo na The Guradian na walikasirika walipogundua kwamba alihusika katika shambulio la 9/11.
Comments
Post a Comment